2015-04-10

Diwani wa CHADEMA Apewa Adhabu ya Kufua Shuka za Wagonjwa Hospitalini na Kuzibua Mitaro ya Barabarani


Diwani wa Kata ya Kasanda wilayani Kakonko, Dickson Barutwa (40) wa Chadema na wenzake watatu, wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kibondo adhabu ya kufua shuka za wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Kakonko na kuzibua mitaro ya barabarani kwa siku 14 baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu.

Baadhi ya makosa hayo yametajwa kuwa ni kuifunga ofisi ya Mtendaji wa Kijiji isivyo halali na kuweka gundi na unga wa ngano kwenye kufuli kwa lengo la kumzuia Mtendaji wa Kijiji asifanye kazi.

Mbali ya Barutwa wengine ni Daudi Obadia (32), Hatari Kasase (33) na Brighton Jona(29), wote wakazi wa kata ya Kasanda, Kakonko. 

Watu hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Erick Marley na kusomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Peter Makalla.

Mwendesha Mashtaka alisema mnamo Novemba 8 mwaka jana, majira ya saa kumi jioni katika kijiji cha Kaziramihunda, watuhumiwa wote kwa pamoja walifika katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho isivyo halali na kuifunga ofisi hiyo kwa kuweka gundi aina ya Super Glue na unga wa ngano kwenye kufuli ili kumzuia Mtendaji asifanye kazi yake.

Inadaiwa watu hao walifikia uamuzi huo kwa madai kuwa hawakuwa wanamtaka Mtendaji huyo wa Kijiji, Amos Peter na kumtishia kumuua.

Kutokana na makosa hayo, Mahakama ya Wilaya ya Kibondo imewahukumu kulipa faini ya Sh 50,000 au kufungwa jela miezi mitano kwa kosa la kufunga Ofisi ya Mtendaji, na pia kulipa faini ya Sh 50,000 au kwenda jela miezi miwili kwa kosa la kufanya fujo. 

Watuhumiwa wote walilipa faini na kuachiwa huru isipokuwa Kasase anayekabiliwa na kesi nyingine ya mauaji, hivyo alirudishwa gerezani.

Aidha, katika kosa la kutishia kuua diwani huyo na wenzake watatu wamehukumiwa adhabu ya kazi za kijamii ambayo ni kufua shuka za wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Kakonko kwa muda wa wiki moja na kuzibua mitaro ya barabara kwa muda wa wiki moja pia.

Tayari diwani huyo na wenzake wameshakabidhiwa katika Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuanza adhabu hiyo. Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walioachiwa huru baada ya kukutwa hawana hatia, ni Boniface Obadia (35) Amos Buseni (33), Majaliwa Charles (24) na Samora Barichako (35), wote wakazi wa kijiji cha Kaziramihunda.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...