2015-04-09

Vigogo Rubada wasimamishwa


 
Waziri wa kilimo, chakula na ushirika  Steven Wassira

SERIKALI imewasimamisha kazi vigogo watatu wa Mamlaka ya Ustawishaji Bonde la Mto Rufiji (Rubada) kwa muda usiofahamika.

Vigogo hao wamesimamishwa kazi baada ya kutuhumiwa kwa ubadhilifu wa zaidi ya Sh bilioni 2.3.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliwataja vigogo hao ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Aloyce Masanja, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji, Tabu Ndatulu na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Filozi Mayayi.

Alisema ubadhilifu huo umebainika baada ya tume iliyoundwa na wizara kwa kushirikiana na Hazina kufanya uchunguzi wa kina.

Wasira alisema viongozi hao wamekuwa wakijihusisha na masuala mbalimbali ya kiuongozi, jambo ambalo kamwe Serikali haiwezi kulivumilia.

Alisema amechukua uamuzi huo wa kinidhamu kwa kutumia mamlaka yake ya waziri mwenye dhamana.

Wasira alisema makosa mengine ya kijinai ameiachia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi.

Alisema vigogo hao walikuwa wakiwatoza fedha watu ambao walikuwa wanataka kuwekeza kwenye kilimo.

“Kibaya, hawa viongozi walikuwa wakiwatapeli wawekezaji kwenye sekta ya kilimo kwa kuwatoza fedha bila kuwaonyesha maeneo ya kulima jambo ambalo lilizua malalamiko makubwa,” alisema Wasira.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 2.7 zilipokewa na maofisa hao kutoka kwa wawekezaji, lakini fedha zilizoonekana kwenye akaunti ni Sh milioni 714.6 wakati Sh bilioni 2.3 hazijulikani zilipo.

Wasira alisema tayari ameiandikia Bodi ya Wakurugenzi ya Rubada ianzishe mchakato wa kujaza nafasi hizo haraka iwezekanavyo ili kazi ziweze kuendelea kama kawaida.

“Maofisa hawa wakuu walikuwa wakijilipa masurufu na baadhi ya fedha zimegundulika kuwekwa kwenye akaunti zao binafsi badala ya ile ya Rubada.

“Fedha za wafanyakazi zaidi ya Sh milioni 58 walizokuwa wakikatwa kwa ajili ya kupelekwa katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ziliishia mifukoni mwao, taratibu za utoaji tenda zilikiukwa, wamefanya watakavyo,” alisema Wasira.

Alisema mfumo mzima wa utendaji wa mamlaka hiyo ulikuwa dhaifu na hakukuwapo na mgawanyo wa kazi, huku maofisa hao wakiidhinisha malipo na kutembea na fedha mifukoni.

Wasira alisema kazi hiyo ilipaswa kufanywa na mhasibu kama utaratibu wa Serikali unavyotaka.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...