Dar es Salaam. Bohari ya Dawa nchini (MSD) imepanga kuanzisha maduka ya dawa katika maeneo yote ya nchi kwa ajili ya kurahisisha usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa pili wa miaka sita unaoanzia 2014 hadi 2020 kwa ajili ya kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa urahisi nchi nzima hadi ngazi ya vituo vya afya.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa MSD, Cosmas Mwaifani alisema jana kuwa mpango huo utakaosimamiwa na ofisi zao za kanda ni sehemu ya mkakati wa kujipanga katika misingi ya kujiendesha kibiashara.
“Ifikapo Januari 30, 2015 bohari itatekeleza mabadiliko makubwa yenye lengo la kuhakikisha dhima ya kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora kwa bei nafuu kwa Watanzania wote inatekelezwa kwa vitendo,” alisema.
Alisema maduka hayo yatafanya kazi saa 24 na kuuza dawa kwa bei nafuu iliyo chini ya bei ya soko na yatatoa huduma kwa watu binafsi na waliopo chini ya utaratibu wa bima za afya watakaokuwa wameandikiwa vyeti vya dawa na vifaa tiba.
Mwaifani alifafanua kwamba maduka hayo yatatoa huduma hizo kwa hospitali binafsi na za Umma.
Alisema hatua hiyo itaongeza wigo wa bohari kusambaza dawa na kuiondoa katika mfumo wa sasa wa kutoa dawa kwa mahitaji maalumu.
Alisema MSD inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutumia wazalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba ili kuepuka gharama ya zaidi ya Dola 100 milioni za Marekani inazotumia kwa mwaka kuagiza asilimia 85 ya dawa na vifaa hivyo nje ya nchi.
Alisema kutokana na hali hiyo kiwango cha upatikanaji wa dawa nchini kimekuwa chini ya asilimia 85 na kuigharimu fedha nyingi kutunza dawa kwa muda mrefu kutokana na kufidia muda mrefu.
a nasiRSS
0 comments:
Post a Comment