Baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wa siasa nchini wamekosoa hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya watuhumiwa wa kashfa ya uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwa kusema kuwa ameshindwa kukata kiu ya watanzania waliotaka kuona anawawajibisha wahusika wote wa sakata hilo.
Wamesema kumfukuza kazi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na kumuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini na Katibu wake hakujaonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Kauli hizi zinakuja siku moja baada ya Rais Kikwete kulihutubia Taifa alipokutana na Wazee wa Mkoa wa Dar Es Salaam zikikosoa uamuzi wake kwa madai kuwa umechukua muda mrefu na hauoneshi dhamira ya kutekeleza maazimio ya Bunge ya kutaka wahusika kuwajibishwa.
Miongoni mwa matarajio ya wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya siasa Marcus Albanie, Tundu Lisu na Said Miraaj Abdullah ni kusikia hatua zilizokwishachukuliwa kulingana na maazimio ya Bunge.
Wakati huo huo, hatua ya Rais Jakaya Kikwete ya kumuondoa katika wadhifa wake aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka kutokana na kupokea fedha zinazohusiana na akaunti ya Tegeta Escrow, baadhi ya wananchi katika jimbo analoliongoza Mbunge huyo la Muleba Kusini mkoani Kagera wametoa maoni yao.
Baadhi yao wamesema uamuzi aliochukua Rais Jakaya Kikwete ni sahihi kwani umezingatia maslahi ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Kufuatia hatua hiyo ya Rais Kikwete, ubishani katika vijiwe mbalimbali mjini Muleba umeshika kasi na baadhi ya wananchi wamejikuta wakilumbana na kutoa tafsiri tofauti tofauti juu ya uamuzi huo.
Nao wakazi wa jiji la Tanga wametoa maoni yao juu ya sakata la Tegeta Escrow wakitaka wahusika wengine wote waliotajwa kwenye kashfa hiyo nao wawajibishwe.
Star TV imetembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Tanga na kukutana na wananchi ambao pamoja na mambo mengine wamepongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Profesa Tibaijuka anakuwa kiongozi wa pili kuachia madaraka, baada ya mwanasheria mkuu wa Serikali Frederick Werema aliyeamua kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa hiyo.
0 comments:
Post a Comment