2015-01-21

Ama Kweli;Siasa imevunja umoja, ikateua wachache kula matunda ya



Hii ni hoja yangu ya siku nyingi. Kila nikifikiria ni jinsi gani tunaweza kujenga jamii bora yenye mshikamano, wazo la hekalu linakuja akilini mwangu. Wale wanaosoma makala zangu, wanajua jinsi ninavyozungumzia jambo hili na kusisitiza umuhimu wake. Ninashindwa kupata neno zuri. Labda wengine wanachanganya hekalu na nyumba za ibada tulizozizoea. Sina maana ya kanisa wala msikiti. Nina maana ya ‘kitu’ cha kuwaunganisha Watanzania wote.


Nafasi isiyokuwa na tabaka, nafasi isiyowatenga matajiri na maskini, waheshimiwa na walalahoi. Nafasi isiyowatenga wanaume na wanawake ni kabila na na dini. Ni mtu gani ana neno zuri zaidi ya hekalu? Basi ajitokeze!


Ninaamini kwamba Watanzania, tunahitaji kitu cha kutuunganisha. Tunahitaji kitu cha kujenga uzalendo. Kitu cha kujenga maadili yetu.


Tunahitaji kitu cha kutufanya kuipenda siyo Tanzania ya leo tu, bali na ya vizazi vijavyo. Nilishaeleza kule nyuma kwamba mifumo yote tuliyonayo sasa hivi haitusaidii. Vyama vya siasa havitusaidii, dini hazitusaidii. Tufanye nini?


Kitabu cha Daktari Adolf Mihanjo, (wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinachohusu falsafa kwa lugha ya Kiswahili kina mambo mengi muhimu kwetu.


“Falsafa na usanifu wa hoja kutoka kwa Wayunani hadi Watanzania (Waafrika)” ni muhimu na msaada mkubwa kwetu.


Zamani za kale nilisoma falsafa kwa Kiingereza, sasa mambo yamebadilika, ni falsafa kwa Kiswahili. Dk Mihanjo amefanya kazi kubwa inayostahili sifa za pekee. Wale waliokuwa wakisema kwamba Kiswahili hakiwezi, sasa watakoma ubishi. Kumbe Kiswahili kinaimudu falsafa ya Wayunani!


Kitabu cha Dk Mihanjo ni msaada mkubwa kwa kila mtu anayethamini kufikiri na kutafakari mambo mbalimbali katika jamii. Katika kitabu hiki mtu anagundua jinsi maendeleo ya mwanadamu yanavyokuja kwa watu kukaa chini kufikiri na kutafakari, na kwamba wanadamu wanasumbuliwa na mambo mbalimbali katika vipindi mbali mbali vya maisha.


Wakati huu sisi tunasumbuliwa na namna ya kujenga jamii iliyo bora, yenye mshikamano, maadili na uzalendo.


Wanafalsafa wa mwanzo wa kule Uyunani walisumbuliwa na kutaka kujua chanzo cha kila kitu. Kwa vile wao walianzisha hoja hiyo na kuitafakari, iliendelea na kufikia kiasi kwamba siyo hoja tena.


Falsafa yao ilisaidia sana maendeleo ya sayansi ya siku hizi. Wanafalsafa hawa wa mwanzoni kabisa ni kina Thales, Anaximander, Anaximenes, Pythagoras, Heraclitus, Permanides na Wanaatomi.


Tukianza na Thales, aliyeishi kati ya mwaka 624 na 546 BC, alifanya kazi ya utafiti wa kisayansi kuhusu asili ya vitu vyote. Vitu vyote vimetengenezwa na nini au ni aina gani ya maada ni chanzo cha kila kitu?

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...