Dar es Salaam. Familia za baadhi ya wafungwa wa dawa za kulevya katika magereza ya China na Hong Kong zimepokea ujumbe wa ndugu zao kutoka magerezani na kueleza chuki yao dhidi ya wafanyabiashara waliowatumbukiza kwenye tatizo hilo.
Wanafamilia hao wameeleza jinsi wanavyoathirika na hali ngumu ya maisha na watoto wa wafungwa hao wanavyoteseka, huku wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wakiendelea kutamba bila kuchukuliwa hatua.
Hadi sasa kuna Watanzania zaidi ya 130 katika magereza ya China na Hong Kong wanaotumikia vifungo kati ya miaka minane na 30 baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa hizo.
Baadhi ya wanafamilia hao walieleza hisia zao baada ya kupokea barua za ndugu zao zilizowasilishwa na Padri John Wootherspoon, Raia wa Australia anayeishi Hong Kong ambaye huwatembelea wafungwa katika magereza hayo.
“Kila wiki lazima Mtanzania aingie katika magereza ya China na Hong Kong, ukiacha mateso makali na kazi ngumu, washtakiwa wanahukumiwa vifungo vya muda mrefu na waliokamatwa China hupata hukumu ya kifo,” alisema Wootherspoon.
Kwa nyakati tofauti wanafamilia watano walilieleza gazeti hili jinsi wanavyoathirika baada ya ndugu zao kufungwa.
Wanafamilia hao, wakiwamo wazazi, watoto, waume au wake za wafungwa walilalamikia hali mbaya ya kiuchumi kwani wale waliofungwa ndiyo walikuwa wanawategemea.
“Mtoto wangu hakuwa na tabia hizo, najua amerubuniwa, sijawahi kumsikia hata siku moja akizungumza kuhusu dawa za kulevya,” alisema mama mmoja, mkazi wa Mbagala ambaye binti yake amefungwa katika gereza la wanawake la Loong Woo, Hong Kong.
Mama huyo alisema binti huyo amemwachia watoto wawili ambao baba zao hawajulikani ,hivyo kubaki na mzigo wa kuwahudumia.
Mwanamke mwingine ambaye mume wake anatumikia kifungo cha miaka 24 katika gereza la Stanley, Hong Kong alisema amelazimika kufanya kazi za ndani ili kujipatia fedha za kuwalea watoto wake watatu.
Alisema amefikia hatua ya kuwadanganya watoto kuwa baba yao anasoma nje ya nchi ili kuhofia wasiathirike kisaikolojia.
Naye mkazi wa Kibaha, alisema anasikitishwa zaidi na hali ilivyo kwa sababu waliomshawishi binti yake abebe dawa hizo wapo mtaani na wanajigamba.
0 comments:
Post a Comment