2015-01-07

Mwaka Huu Ni Shida:Mbinu za fitina hazitatupatia rais bora


Vita ya makundi vimeitesa CCM kwa muda mrefu. Wakati vita vya makundi ya 2005 vinaelekea kufifia, sasa kumezuka vita vya makundi mapya ya 2015 ambavyo navyo si haba kwa fitina na kuhujumiana. 



CCM imejaribu kulidhibiti tatizo la vita vya makundi ya urais, lakini kila kukicha makundi hayo yanaibuka na mbinu na mikakati mipya.


Katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa awamu ya nne kuna watu walianza fitina zao kwamba Waziri Mkuu Lowassa, alikuwa anamfunika Kikwete.


Juu ya yote hayo kulikuwa na kundi jingine la fitina ambalo lilikuwa halijitokezi hadharani lakini linafanya kazi chinichini kuharibu haiba ya kiongozi au viongozi wanayemlenga.


Hili kundi limebatizwa kuwa kundi la Brutus. Brutus alikuwa mwandani wa Julius Kaizari, ambaye alipigana vita na kujenga himaya ya Kirumi. Aliwaletea utajiri mkubwa watu wa Roma hasa wale wa matabaka ya chini na matabaka ya kati. 



Mipango ya kumuua Julius Kaizari ilitokana na watu wenye kundi moja ambalo walizidiwa na tamaa ya uongozi na mali.


Historia ya Roma inatuambia kwamba baada ya Kaizari kuuawa, Roma haikuwa na amani tena. Kulitokea vita vya wenyewe kwa wenyewe na mwisho wa himaya ya Roma ulikuwa umewadia.


Kundi la Brutus la hapa kwetu mara zote mkakati wake ni kuonyesha uongozi wa juu kwamba unazo habari nyeti kuhusu mipango ya baadhi ya viongozi wenye uchu wa madaraka ambao wanataka kuhujumu mipango ya chama au Serikali.


Kundi hilo ni mojawapo ya makundi ambayo yalikuwa yanavujisha habari za vikao nyeti vya serikali na chama kwa vyombo vya habari kujaribu kuharibu sifa ya viongozi wasiowapenda.


Wakati wa sakata la Richmond, kulivujishwa habari kwamba kundi la Lowassa, ambaye aliachia ngazi kama Waziri Mkuu, lilikuwa na mpango wa kutaka kumwondoa mwenyekiti wa CCM kwenye nafasi hiyo na badala yake wamweke mtu wao kama ilivyofanyika Afrika ya Kusini.


Kilichofanyika Afrika Kusini ni Zuma na kundi lake, akiwamo mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ANC, Julius Malema walipiga kampeni ya nguvu dhidi ya Rais Thabo Mbeki na wakamlazimisha kujiuzulu nafasi ya uenyekiti na akapoteza nafasi ya urais wa nchi. Hoja za namna hiyo zilikuja kujitokeza katika Mkutano Mkuu wa CCM wa mwaka 2011. Kwa CCM taratibu zake za kumpata mwenyekiti wa chama ni tofauti na taratibu za Afrika ya Kusini.


Kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa, habari ya kundi moja kutaka kumwondoa mwenyekiti wa chama ziligonga mwamba kutokana na taratibu za kikanuni ambazo hazikuwapa mamlaka makuu ya kufanya hayo. Ilionekana haiwezekani kufanyika kwani mwenyekiti anachaguliwa na Mkutano Mkuu wa chama.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...