2015-01-19

Ni hatari sana:Mbunge wa Mbinga akalia kuti kavu

 

Wafanyabiashara wadai ameshindwa kuwatetea bungeni katika suala la ongezeko la kodi.

Mbinga Wafanyabiashara wilayani hapa, wametishia kutomchagua Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kile walichodai ameshindwa kuwatetea bungeni na badala yake ameunga mkono ongezeko la kodi la asilimia 100.

Wakizungumza wakati wa kikao cha wafanyabiashara na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mbinga, mmoja wa wafanyabiashara hao, Benedict Lwena alisema wameumizwa na mbunge wao kushindwa kuwatetea kuhusu suala hilo. 
“Hatukumtuma bungeni kwenda kulala, bali kutuwakilisha, kutokana na kutugeuka nasi tumejipanga kumwangusha kwani hatuwezi kuwa na mbunge asiyejali kero za wananchi wake,” alisema Lwena.

Mfanyabiashara mwingine, Ally Mbunda alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba kukutana na mbunge huyo ili waweze kuzungumzia kero zinazowasumbua lakini amekuwa akisema amebanwa na majukumu mengine.

Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana, mbunge huyo alikiri kusikia malalamiko hayo lakini akashangazwa na taarifa hizo akisema, tangu kikao kilipomalizika hakuna viongozi wala wafanyabiashara waliomfuata kumweleza hatua zilizofikiwa juu ya kikao hicho. 


Alisema anashangaa kwa nini malalamiko hayo yanatokea kipindi hiki cha kampeni, “Siyo wafanyabiashara peke yao wanaopiga kura, kwanza sheria inapitishwa na wabunge wote na inatumika nchi nzima hivyo sioni haja ya wao kuniadhibu.”

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...