2015-02-25

CCM yajichimbia kusuka ripoti ya kina Lowassa

kikwete
Na Esther Mbussi, Dar es Salaam
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), itategua kitendawili dhidi ya makada sita waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa madai ya kuanza kampeni za kuwania urais ndani ya chama hicho kabla ya wakati.

Kutokana na hatua hiyo katika kikao hicho kitakachofanyika Februari 28, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, Philip Mangula, atawasilisha ripoti yake ya tathmini dhidi ya makada hao kama walitekeleza adhabu waliyopewa na chama ama la.

Makada hao walitakiwa kutojihusisha na harakati zozote zinazoashiria kampeni ya kushawishi kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, taarifa yake ya tathmini ndiyo inaweza kutoa dira na hatima ya makada hao ambao walipewa adhabu hiyo Februari 18, mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilieleza kikao hicho cha CC kitafanyika jijini Dar es Salaam chini ya 
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CCM ambayo haikueleza ajenda za kikao hicho, vikao vya maandalizi vinaendelea na kazi yake.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM Lumumba, kiliiambia MTANZANIA kuwa kwa siku kadhaa Kamati ya Mangula imekuwa ikifanya vikao vyake hadi usiku wa manane, ikiwa pamoja na kupitia majalada mbalimbali dhidi ya makada hao yaliyokuwa yamefunguliwa katika kila mkoa.

Makada ambao waliangukiwa na adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, 
Steven Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

“Kikao hiki cha Kamati Kuu ndiyo kitatoa mwelekeo na hatima ya wana CCM waliofungiwa, maana Mangula atawasilisha ripoti ya tathmini mbele ya kikao kwa uamuzi zaidi.

“Ikiwa kikao kitaridhika na mienendo yao, wapo watakaotangazwa kuwa huru, lakini wale ambao bado walikuwa wakiendelea na harakati za kufanya kampeni ya kushawishi 
kinyume cha utaratibu wanaweza kuangukiwa na mkono wa chama ikiwamo kupoteza sifa za kuwania urais mwaka huu,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Chanzo hicho kilisema mbali na Mangula kuwasilisha ripoti, pia kikao hicho kitajadili hatua za kuchukuliwa dhidi ya vigogo 
walioitwa na chama kujieleza kutokana na kupokea fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Makada ambao waliwekwa kikaangoni kutokana na kupokea mgawo huo, ni 
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, 
Wiliam Ngeleja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.
Uamuzi huo umekuja baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM, iliyokutana Januari 13, mwaka huu visiwani Zanzibar, ambapo 
pamoja na mambo mengine, iliagiza kuhojiwa kwa makada wake hao wenye nafasi ndani ya chama kama njia ya kujenga nidhamu, maadili na uwajibikaji kwa masilahi ya chama na umma.

Katika kikao hicho, makada hao waliopokea mgawo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, watatakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu walivyopokea fedha hizo.

Mbali na hilo, vigogo hao ambao walifunguliwa majalada na chama kupitia Idara ya Maadili ya CCM chini ya mkuu wake, Masudi Mbengula, watatakiwa kutoa utetezi wao juu ya kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu na chama kwa kukiuka maadili.

Katika mgawo huo wa Escrow, Profesa Tibaijuka alipokea Sh bilioni 1.6, Chenge naye akipokea kiasi kama hicho, huku Ngeleja akipokea Sh milioni 40.4.

Chenge na Ngeleja wote ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), ambapo kwa mujibu wa mazimio ya Kamati Kuu iliyokaa Zanzibar, makada hao pamoja na Tibaijuka ikiwa watakutwa na hatia wataadhibiwa, ikiwamo kuvuliwa nyadhifa zao ndani ya chama.

Mbali na CC kupokea taarifa ya Kamati ya Mangula, pia itajadili na kupanga ratiba ya kuwapata wagombea wa nafasi ya urais, wabunge na madiwani ndani ya chama hicho kabla ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Taifa.

“CC itatoa utaratibu mzima wa ratiba za vikao vya uteuzi kwa wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, lakini pia itapokea taarifa ya kuanza kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mfumo wa elektroniki, maarufu BVR ambao umeanza juzi mkoani Njombe.

“Katika kikao kilichopita cha Kamati Kuu, ilipitishwa ratiba ya shughuli mbalimbali za chama kwa mwaka 2015… ila ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola utapangwa na kikao hiki cha Februari 28, hapo ndiyo tutaanza kusikia nchi ikilipuka na hata kuona nguvu ya CCM,” kilisema chanzo hicho.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...