Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kihenya Kihenya.
Wanafunzi wawili wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Unity, iliyopo Chamazi, eneo la Mbagala, Manispaa ya Temeke, wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa darasa la shule hiyo uliogongwa na gari.
Kadhalika, wanafunzi watatu wamejeruhiwa baada ya kijana wa kazi wa mmiliki wa shule hiyo, ambaye siyo dereva kujaribu kuendesha gari na kuparamia darasa hilo na sehemu ya ukuta kuwaangukia wanafunzi waliokuwa darasani wakiendelea na masomo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kihenya Kihenya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Februari 03, mwaka huu, majira ya saa 2:30 asubuhi, na wanafunzi wawili wamefariki na watatu kujeruhiwa na kwamba mtuhumiwa wa tukio hilo anashikiliwa na jeshi la Polisi.
“Wanafunzi watatu wametibiwa katika hospitali ya Mbagala na wameruhisiwa baada ya kupata nafuu,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda huyo alipotakiwa kutaja majina ya wanafunzi hao na mtuhumiwa huyo, alisema yupo nje ya ofisi hawezi kukumbuka majina yote.
NIPASHE ilifika eneo la tukio na kukuta geti la kuingia kwenye shule hiyo iliyopo kwenye eneo moja na nyumba ya mmiliki ambaye jina halijafahamika, na kuona ukuta ukiwa umeanguka.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema chanzo cha ukuta huo kuanguka ni kijana mmoja wa familia hiyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30, ambaye ni mmoja wa wanafamilia ya nyumba hiyo, aliyeendesha gari aina ya Rav 4 ambalo liliparamia ukuta huo.
Mashuhuda hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema, tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30 asubuhi, wakati wanafunzi hao wakiwa darasani.
“Nikiwa bafuni naoga nilisikia kishindo kikubwa, nilitoka kwa kasi hadi eneo la shule na kukuta ukuta umeanguka umelalia watoto, tulianza kuwaokoa na tulifanikiwa kuwatoa watano kati yao wawili walikuwa wamelaliwa na matofali na wana hali mbaya,” alibainisha na kuongeza:
“Tulijiuliza nini kilitokea na baadaye tulimuona kijana aliyeendesha gari akiwa ndani ya gari, tulimtoa akiwa hajitambui na gari imeharibika vibaya, tulimpepea hadi akazinguka, tuliwajulisha polisi na baadaye kupelekwa kituo kikuu cha polisi cha Kizuiani,”.
Baba wa mtoto wa kiume Isiaka Mketo (12), aliyefariki katika tukio hilo, Twaha Mketo, akizungumza na NIPASHE wakati wa maziko ya mwanaye, alisema alirejea nyumbani majira ya saa mbili asubuhi na kujisikia mwili mzito na baadaye aliingilia ndani na kupumzika, lakini ndani ya muda mfupi alipigiwa simu na mkewe kuwa mtoto anaumwa sana yupo hospitalini.
“Nilikwenda hospitali ya Zakhem na kuwakuta walimu ambao waliniita pembeni na kunieleza kuwa watoto watano waliangukiwa na ukuta na mwanangu na mwingine wa kike wamefariki…niliumia sana, nililia sana, lakini ndiyo limeshatokea nimelipokea na jana nimemzika mwanangu,” alisema.
Alisema walimu walimueleza kuwa wanafunzi walikuwa darasani gari likagonga ukuta wa darasa lao na ukuta kuwaangukia na kwa bahati mbaya wawili walifariki.
Mwanafunzi wa kike aliyefariki katika tukio hilo, amejulikana kwa jina moja la Kulthum, wa eneo la Charambe, Magengeni.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa majeruhi akiwa na mzazi wake katika mazishi ya Isiaka, alisema alikisia kishindo kikubwa na ghafla matofali yakawafukia kwa muda na kwa kuwa alikuwa pembeni kidogo alijeruhiwa kichwani.
“Watu walikuja haraka kutusaidia, nilimuona Isiaka akiwa amelala aliitwa, lakini hakuitika…nafikiri alishakufa,” alisema huku akibubujikwa na machozi.
Mkuu wa shule hiyo, alipotafutwa kwa simu iliita bila kupokewa na baadaye ilizimwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa na NIPASHE ilifika shuleni na kukuta ulinzi umeimarishwa.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment