Mchumi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Brown Kajange (42) amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kujibu mashitaka mawili, likiwamo la shambulio la aibu kwa kumshika matiti mwanamke bila ridhaa yake.
Karani wa Mahakama hiyo, Blanka Shao alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Matrona Luanda kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 16, mwaka huu katika eneo la kuuzia samaki la Feri Kivukoni wilaya ya Ilala.
Shao alidai siku ya tukio saa 6 mchana katika eneo hilo, mshtakiwa alimshika matiti Queensia Fusi bila ridhaa yake huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa shtaka la pili, mshtakiwa alimpiga ngumi mlalamikaji katika jicho la kushoto na kusababisha maumivu makali katika sehemu hiyo. Mshtakiwa alikana mashtaka na Hakimu Luanda aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, mwaka huu itakapotajwa.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka serikali ya mtaa, atakayesaini bondi ya Sh 300,000.
0 comments:
Post a Comment