2015-02-21

Rais Kikwete aapishwa kuwa mwenyekiti EAC



Da/Arusha. Rais Jakaya Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akichukua jukumu hilo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyemaliza muda wake.


Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika mkutano wa 16 wa wakuu hao wa nchi hizo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Jomo Kenyatta.


Jana, nchi hizo zilizindua mfumo wa mawasiliano ya pamoja ambapo Rais Kikwete aliwasiliana na Balozi Sefue na kuzungumza naye mambo machache.


Marais wengine wa nchi hizo wanachama pia walifanya hivyo kwa kuwasiliana na mataifa yao.


Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilizindua mfumo huo ambao utaziwezesha nchi wanachama kupunguza gharama za uendeshaji wa mikutano baina ya wajumbe wao. Awali, wajumbe walilazimika kusafiri na kukutana sehemu moja.


Akielezea mfumo huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Jamii wa wizara hiyo, Eliabi Chodota alisema kuwa, utasaidia kupunguza gharama katika mikutano mbalimbali inayofanyika baina ya wajumbe wa nchi wanachama.


“Mfumo huu utaondoa haja ya wajumbe kukutana. Marais, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na wafanyakazi wa Serikali wataendesha mikutano yao bila ya kukutana. Hii itapunguza matumizi ya fedha kwa ajili ya kujikimu na bajeti nyingine za mikutano,” alisema Chodota.


Alifafanua kuwa wanyakazi wa taasisi mbalimbali zinazoshirikiana wataweza kutatua matatizo yatakayojitokeza kwa kutumia mfumo huo jambo litakaloongeza ufanisi katika utatuzi wa kero ndogo ndogo zinazowakumba wananchi wa mataifa wanachama.


Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hafahamu sababu ya Kenya kuzuia magari yenye usajili wa Tanzania kufika na kuingia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini humo.


Balozi Sefue alisema hayo alipozungumza na gazeti hili katika ofisi za Wizara ya Afrika Mashariki (EAC), alikohudhuria uzinduzi wa mfumo wa kuendesha mikutano kwa njia ya video (video conferencing) uliokuwa ukifanyika Kenya.


Alisema Serikali inashangaa kuona zuio hilo linafanyika wakati mkataba wa ushirikiano katika sekta ya utalii baina ya nchi hizi mbili ulisainiwa mwaka 1985 na kubainisha vipengele vitakavyohusika.


“Mazungumzo yanaendelea ili kurekebisha tatizo lililojitokeza. Tumeshtushwa na zuio hilo licha ya kuwapo kwa mkataba unaoruhusu jambo hilo. Mpaka sasa hawajatuambia tatizo ni nini lililowafanya wazuie magari yetu,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...