PEPO la ugomvi linazidi kumuandama staa wa Bongo Fleva, Khaleed Mohamed ‘TID’, baada ya kusakwa na jeshi la polisi kwa kosa la kumjeruhi mtu mwishoni mwa wiki iliyopita, msanii huyo ametengeneza kicha cha habari kwa mara nyingine akidaiwa kumpiga meneja wake aliyefahamika kwa jina la Tall Mnyama.
Katika tukio la awali, TID alidaiwa kutembeza kichapo na kumjeruhi James Richard, mkazi wa Jiji la Dar kwa kosa alilodai kuwa ni kupaki gari kwenye eneo lake, maeneo ya nyumbani kwa msanii huyo, Kinondoni-Sterio jijini Dar.
Tukio la kumpiga meneja wake, TID anadaiwa kulifanya katika Hotel ya Element, Oysterbay ambapo inaelezwa kuwa msanii huyo alifika hotelini hapo akiwa na wapambe wake na alipomkuta meneja huyo, alibishana naye kwa muda mfupi kisha kumzaba kibao.
“Alimkuta mwenzake (Tall) kaka sehemu, akamsemesha na alipojibu tu akamzaba kofi, lakini huyu meneja wake alikuwa mstaarabu, hakumlipizia. Baada ya tukio hilo TID alitokomea na kama unavyojua sasa hivi anaishi kama digidigi, mbaya zaidi watu wanasema asipompiga mtu hasikii raha,” kilidai chanzo chetu.
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ‘ubuyu’ kuwa, meneja huyo baada ya kupokea kipigo hicho, alikwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Oysterbay kilicho chini ya Camillius Wambura (pichani) ambapo lilifunguliwa jarada lililosomeka; OB/RB/3922/2015/TAARIFA.
RPC Camillius Wambura.
Mwanahabari wetu alipomtafuta meneja huyo kuhusiana na tukio hilo, alikiri kuwa limemtokea lakini akasema hakutaka kulivalia njuga lakini alichokifanya ni kutoa taarifa polisi ili endapo atarudia, amchukulie hatua kali zaidi za kisheria.
“Ni kweli TID alinishambulia kwa kunipiga kibao, iliniuma sana lakini nimeamua kumsamehe, nilichokifanya ni kutoa taarifa polisi ili kama atarudia nimfikishe katika vyombo husika,” alisema meneja huyo.
Jitihada za kumpata TID ili aweze kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani.Jitihanada za kumpata Wambura hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa kwa siku ya juzi.
0 comments:
Post a Comment