HALI ya siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kuwa tete baada ya makundi mbalimbali ya jamii kwenda kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa achukue fomu ya kugombea urais.
Hali hiyo imedhihirika baada ya makada wa chama hicho kuanza kuvurugana kwa kutoa kauli zinazopingana juu ya wanaomtembelea Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, kuwataka wajumbe wa Baraza la Wazazi la chama hicho kuomba radhi kwa kitendo chao cha kwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma na kumtaka agombee urais.
Pamoja na Bulembo kutoa kauli hiyo, wajumbe hao wamesema hawako tayari kuomba radhi kwa sababu hawaoni sababu ya kufanya hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, wajumbe hao wa Baraza la Wazazi wa CCM, walisema hawataomba radhi kama walivyotakiwa na Bulembo kwa vile walikwenda kwa Lowassa kwa hiyari yao na kwa mapenzi yao binafsi.
Katika mazungumzo yake, Lupenza alisema viongozi walioratibu ziara hiyo ni pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang, Vioroka Kajoro na Mjumbe wa baraza hilo Mkoa wa Morogoro, Jackline Ngonyani pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mkoa wa Dodoma, Dk. Damas Mukassa.
Alisema yeye hakushawishiwa na mtu yeyote kwenda kwa Lowassa ila aliwasikia viongozi hao wakizungumzia juu ya ziara hiyo na kuwataka waweke jina lake kwenye orodha ya watakaokwenda kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani.
“Niliwasikia wakisema kwa mzee ni saa tatu, nikawauliza mnataka kwenda wapi, wakaniambia wanataka kwenda kumsalimia Lowassa, nikawaambia waniandike na mimi jina.
“Kwa hiyo hakuna mtu aliyenishinikiza na hata siku hiyo ya safari, hakuna aliyenikumbusha, kwanza waliniacha nikaenda kwa pikipiki nikiwa nimechelewa,” alisema Lupenza na kuongeza:
“Ngonyani ambaye amekaririwa na vyombo vya habari akisema alishinikizwa kwenda kwa Lowassa, nilimkuta akiwa nyumbani kwa Lowassa akiwa amekaa kwenye viti vya mbele kabisa.
“Hata wakati wa kupiga picha ulipofika, Ngonyani huyo huyo ambaye sasa ametugeuka, aliwataka wajumbe wengine wote wakae mbali aweze kupiga picha yeye na Lowassa peke yao.
“Yaani hata wakati tunajitambulisha huyo huyo Ngonyani alisema ametumwa na watu wa Ruvuma kumletea salamu Lowassa, kwamba wanamsalimia, sasa anageukaje tena?”
Profesa Maji Marefu
Kwa upande wake, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani ambaye ni maarufu kwa jina la Profesa Maji Marefu, alikana kuratibu safari hiyo kama ilivyodaiwa na kueleza kuwa alishirikishwa katika dakika za mwisho na akaamua kwenda.
“Wanaojitoa katika ziara hiyo hivi sasa nadhani walifikiri wakienda pale watapewa fedha ama magari. Mimi nimekaa kwenye hii jumuiya kwa miaka 15 sasa, siko tayari kuchaguliwa kiongozi, marafiki wala maadui. Siko tayari kuomba radhi kwa sababu sina kosa nililotenda, nasema sitaomba radhi,”alisema Ngonyani.
Naye Dk. Mukassa alisema yeye aliratibu ziara hiyo kama mwenyeji wa Mkoa wa Dodoma ambaye anapafahamu nyumbani kwa Lowassa.
Alisema Sh 600,000 walizozitoa kwa ajili ya Lowassa kuchukulia fomu ya kugombea urais, zimetokana na michango yao wenyewe kama wanachama wa kikundi cha kusaidia wajumbe wa jumuiya hiyo.
“Fedha zile hazikutoka kwenye jumuiya ya chama wala hakuna aliyekwenda pale kuwakilisha jumuiya na nilieleza pale,”alisema.
Nape na Lowassa
Wakati hayo yakiendelea, jana Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akiwa wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, alitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu hatua inayoendelea ya kushawishi makada wa CCM kuwania urais. Alisema kinachoendelea hivi sasa mjini Dodoma kwa makundi tofauti kwenda kwa Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi na kwamba ni matendo ya wazi ya kampeni.
Kutokana na hali hiyo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, anajua adhabu yake kwa matendo hayo kwamba anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea kupitia CCM.
Alisema Lowasa ni miongoni mwa wana CCM sita waliopewa adhabu na CCM mwaka mmoja uliopita na kwamba mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
Kwa mujibu wa Nape yanayoendelea hivi sasa ni dhahili kuwa ni kiburi kisicho na maana dhidi ya CCM.
“Lowassa anajua utaratibu wa chama katika kuwapata wagombea kwa ngazi mbalimbali, kuanzia udiwani mpaka urais. Hivyo, kuendelea na matendo ambayo yanatafsiri ya wazi kuwa ni kampeni ni kiburi cha wazi.
“Labda dhamira iwe ni kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya urais kupitia chama kingine na si CCM.
“Ni vema wagombea wa ngazi mbalimbali wazingatie Katiba na kanuni za chama wasiingie kwenye kundi la kutokuwa na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea udiwani, ubunge na urais.
“ Tunasisitiza na kukumbusha kwamba wale wote wenye nia ya kugombea kupitia chama chetu waheshimu kanuni na tararibu za kupata ridhaa kugombea kwa ngazi ya chama chetu,”alisema Nape.
Kwa siku kadhaa sasa makundi mbalimbali yamekuwa yakimiminika nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma na Arusha kwa lengo la kumshawishi muda ukifika achukue fomu ya kuwania urais kupitia CCM.
Mbali na vikundi hivyo, pia masheikh 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani nao wamekwisha kwenda nyumbani kwa Lowassa mkoani Dodoma kwa nia hiyo hiyo.
Juzi, baadhi ya wachungaji wa madhehebu mbalimbali walikwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma na kumtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani agombee urais muda utakapofika.
Akizungumza na makundi hayo kwa nyakati tofauti, Lowassa alisema anafarijika kuona makundi mbalimbali yakifika nyumbani kwake kumshawishi. Pia alisema miongoni mwa makundi hayo, hakuna kundi hata moja alilolituma na kutoa fedha wamfuate nyumbani kwake.
0 comments:
Post a Comment