SAKATA la uongozi ndani ya Chama cha Mabadiliko na Uwazi (ACT-Tanzania), limeendelea kuchukua sura mpya baada ya uongozi uliodaiwa kuvuliwa madaraka, kudai Bw. Zitto Kabwe ndiye aliyesababisha mgogoro katika chama chao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Kadawi Limbu alisema chanzo cha mgogoro unaoendelea katika chama hicho ni Bw. Kabwe ambaye awali hakuwa mwanachama halali; lakini alipanga mikakati yote nje ya chama.
Alisema mikakati mingi ya chama hicho ilipangwa nyumbani kwa Bw. Kabwe na watu watatu akiwemo Profesa Kitila Mkumbo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Samson Mwigamba bila yeye kama kiongozi (Limbu) kujulishwa.
"Nipo tayari kufa hadi haki ipatikane, mimi ndiye kiongozi wa ACT-Tanzania, mara ya mwisho kuwasiliana na Bw. Kabwe ni Desemba 10, 2014, barua kutoka kwa Msajili Siasa ya Februari 27, 2015 kwenda kwa Katibu Mkuu wa chama, alisema yeye ametoa ushauri si maelekezo.
"Ushauri wake tunaweza kuufanyia kazi kwenye vikao, lakini imechukuliwa tofauti na kuonekana Msajili amebariki kufanya walichofanya...haiwezekani uchaguzi wa mikoani ufanyike na watu watatu, mimi ni mti mkavu ndani ya ACT, lakini Kabwe na Selemani Msindi (Afande Sele) ni miti mibichi," alisema.
Bw. Limbu aliongeza kuwa, kadi yake ni namba moja ndani ya ACT, hivyo ndiye mwanzilishi wa chama hicho ambapo Bw. Kabwe ameingia siku chache zilizopita na Katiba ya chama hairuhusu mwanachama kugombea uongozi hadi afikishe miezi sita ndio apate uongozi.
Alisema kwa sasa wamefungua kesi namba 17 ya mwaka 2015; hivyo kama ACT-Tanzania wataendelea na taratibu za
kuchagua viongozi ndani ya chama wataishia njiani hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
"Kabwe hawezi kuhamia kwenye chama ambacho hakina Mwenyekiti na Makamu...yupo Katibu peke yake, tunamwonya aingie kwenye chama; lakini hatutaki migogoro," alisema.
Aliongeza kuwa, hivi sasa wako mbioni kuhamisha ofisi za chama hicho kwani zipo nyumbani kwa mtu ili waendelee na kazi ndio maana mgogoro ulivyotokea waliamua kutokwenda ofisini ili kuepusha madhara ambayo yangeweza kutokea.
"Licha ya Kabwe kudai ni mzalendo, lazima ajipime kwanza na wenzake kwani anachokifanya si sahihi, sifa ya mzalendo
ni mtu kuogopa kitu cha watu wengine, haiwezekani mtu afanye maamuzi nje ya chama," alisema Bw. Limbu.
Akijibu tuhuma hizo, Bw. Mwigamba alisema Msajili wa Vyama vya Siasa alitoa ushauri kwao ili kumaliza mgogoro uliopo kwa njia ya amani si vinginevyo.
Akizungumzia kesi iliyopo mahakamani, alisema si kwamba Bw. Limbu na wenzake wamemshtaki Katibu Mkuu, bali walioshtakiwa ni wengine ndani ya chama.
"Tunamtambua Limbu kama mwanachama wetu halali lakini si kiongozi wala Mwenyekiti wa chama, tunamkaribisha aweze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
"Kuhusu Kabwe, sisi hatuwakatai wanachama bali tunamshukuru kwa kuja na kutuongezea wanachama wapya 12 waliojiunga kwa siku moja," alisema.
Bw. Mwigamba alisema Bw. Limbu na wenzake walikuwa hawataki uchaguzi ufanyike ndani ya chama jambo ambalo
haliwezekani kwani chama kinaweza kikafutwa na hayo anayosema ni yake; lakini kila kitu kipo wazi.
0 comments:
Post a Comment