Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damiani Lubuva akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waratibu wa uandikishaji wa mikoa na maofisa wa uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Picha na Venance Nestory
Awataka wachunge ndimi zao, asema kauli wazitoazo kuhusu BVR zinaweza kusababisha machafuko nchini.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amewashukia viongozi wa kisiasa, akiwataka kuacha kutumia nafasi zao kuingilia mchakato wa uandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa kutumia vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR), kwani zinaweza kuleta machafuko makubwa nchini.
Jaji Lubuva aliyasema hayo jana Dar es Salaa alipokuwa akifungua mkutano wa waratibu wa uandikishaji wa mikoa na maofisa waandikishaji kuhusu uboreshaji wa daftari hilo linalotarajia kutumia Aprili 30, mwaka huu, wakati wa kura ya maoni ya kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Akitoa ufafanuzi wa kina juu ya mashine hizo, alisema tume imejipanga kuhakikisha uandikishaji unakwenda kama ulivyopangwa na kusisitiza kwamba hakuna mtu yeyote mwenye sifa ya kuandikishwa atakayeachwa katika mchakato huo.
“Viongozi wa siasa wasitumie mwamvuli wa BVR kutaka kufanya fujo bali watumie nafasi hii kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha.
Kuhusu maandalizi ya kuanza uandikishaji kwa Mkoa wa Njombe Jumatatu ijayo alisema: “Kila kitu kimekamilika, mashine zote zimeshafika Njombe na tunachosubiri ni kuanza uandikishaji katika vituo 44 na kila halmashauri zitatumika siku 28, kituo kimoja kitatumia siku saba.”
Akizungumzia mashine za BVR 7750 ambazo hazijafika alisema: “Serikali imeshazilipia, tunatarajia zitafika wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi ujao.”
zitakapo fika tutawatangazia ratiba kamili ya mikoa mingine.”
Viongozi wa vyama vya siasa wakizungumzia kauli ya Jaji Lubuva walisema endapo mchakato wa uandikishaji utakwenda vizuri, hakuna atakayesababisha machafuko.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema: “Tunachokipinga sisi ni kuanza kuandikisha kwa vipande vipande, mara Njombe, Mtwara, kwa hali hii haturidhiki.
“BVR italetaje fujo au machafuko endapo uandikishaji utakwenda vizuri, lakini kama utakwenda vibaya hapo ndipo fujo na machafuko yanaweza kutokea.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema: “Ninachohofia mimi ni kama muda uliopangwa unatosha na hivyo vifaa kama vitafika kwa wakati.
“Hakuna mwenyekiti wa chama chochote anayeweza kusababisha vurugu kama mchakato mzima wa uandikishaji utakwenda vizuri, tume itekeleze watu wote waandikishwe.”
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment