2015-02-21

EWURA Yapitisha Kanuni za Tozo Huduma ya Gesi



Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imepitisha maombi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu kanuni za tozo za huduma ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini, Mkurugenzi Mkuu EWURA, Felix Ngamlagosi alisema TPDC iliiomba Ewura kuidhinisha vipengele vya kanuni ya kurekebisha tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia itumike kwa miaka 20 hadi mwaka 2034, tozo kwa huduma ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia iwe katika dola za Marekani.

Pia waliomba faida kwenye mtaji ya asilimia 18 na muundo wa mtaji wa asilimia 50 mkopo na asilimia 50 fedha za TPDC na mwezi Septemba kila mwaka wa tatu utakuwa ni mwezi ambao marekebisho ya tozo kwa miaka mitatu inayofuata yatawasilishwa kwa EWURA. 

Alisema bodi ya EWURA ilijadili ombi la TPDC na kufikia maamuzi ya kipindi kifupi cha miezi mitatu ambacho TPDC itakitumia kukamilisha ujenzi na kuwasilisha gharama halisi ambayo EWURA iliyahoji.

Aliongeza kuwa maamuzi yaliyotolewa na EWURA ni kanuni ya kukokotoa tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia iliyoombwa ilirekebishwe na kupitishwa ili itumike kwa miaka 20 kuanzia mwezi Aprili mwaka huu na kurekebishwa kila baada ya miaka mitano.

Pia gharama za mradi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zilizopitishwa ni sawa na dola za Marekani milioni 1,331,51 ambapo gharama hizi zitabaki hivyo hadi mwezi Juni hadi gharama halisi za mradi zitakapojulikana na kufungwa.

Alisema maamuzi mengine ni gharama za uendeshaji zitakuwa sawa na dola za Marekani milioni 241.58 kwa mwaka na muundo wa mtaji kwa ajili ya mradi wa bomba la gesi asilia Mtwara hadi Dar es Salaam litagharamiwa kwa mkopo wa kiasi cha asilimia 75 na mtaji wa TPDC.

Aidha mradi wa miundombinu ya bomba na mitambo ya kuchakata gesi asilia utatekelezwa kipindi cha miaka 20 kutoka tarehe ya uzinduzi wake na tozo ya kuchakata gesi italipwa kwa Shilingi ya Tanzania kwa kiasi sawa na jumla ya dola za Marekani 2.14 kwa uniti ambapo tozo ya kuchakata gesi itakuwa dola za Marekani 0.95 kwa uniti na tozo ya kusafirisha gesi itakuwa dola za Marekani 1.19 kwa uniti. 

Pamoja na maamuzi hayo pia EWURA imewataka TPDC kutimiza masharti ya kuzingatia kanuni za ushindani kama zilivyoainishwa katika sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na kuiarifu Ewura kila watakapofanya manunuzi ya thamani yanayozidi dola za Marekani milioni tano.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...