YALE mapigano yaliyotikisa Mapango ya Amboni jijini Tanga kwa saa 48 kati ya watu wanaodaiwa na wananchi kuwa ni magaidi na majeshi ya ulinzi ya Tanzania bado ngoma nzito kufuatia baadhi ya wananchi kusema mengine mapya wanayoyajua kuhusu magaidi hao, Uwazi limechimba na kuchimbua.
Polisi wakipambana na magaidi hao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa Vijiji vya Mafuriko, Mikocheni, Majimoto, Kilomoni na Amboni yenyewe, wanaamini wahalifu hao ni makomandoo wazuri na waliishi kwenye mapango hayo wakijua siku wakivamiwa watapambana vikali.
KWA NINI MAKOMANDOO?
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Majimoto alisema kwa jinsi watu hao walivyofanikiwa kutoweka katika mazingira tata huku wakiwa salama haingii akilini kwamba ni wapiganaji wenye mafunzo ya kawaida.
“Wakati risasi zinapigwa na serikali inatuambia tuchukue tahadhari kwa mtu tusiyemjua tumtolee taarifa tuliamini lazima watakamatwa hata kama si wote. Lakini tulipoambia hali imetulia lakini hajakamatwa hata mmoja tulishangaa sana,” alisema mkazi huyo akiomba asitaje jina lake.
KUMBE WAPO TANGU 2013!
Akizungumza na Uwazi, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Amboni aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan alisema magaidi hao walipiga kambi kwenye mapango hayo tangu mwaka 2013.
“Sisi tulianza kuwaona mwaka 2013, sikumbuki mwezi. Lakini walionekana kama wachimba kokoto ndiyo maana walidumu kwa muda wote huo. Pale kuna sehemu watu wanachimba kokoto.”
ILIKUWA KAMA KWAO
“Naweza kusema walipatawala pale kwani ilikuwa kukicha, wengine walikuwa wakienda mjini wengine wanashinda palepale. Haikuwa rahisi kudhani ni magaidi,” alisema Hassan.
MAMBO MATATU YAIBUKA
Hata hivyo, wananchi hao ambao wanasema mpaka sasa hawana amani licha ya kuwepo kwa askari polisi kila kona kulinda, walisema kuna mambo matano ambayo polisi wamekaa kimya kuyatolea ufafanuzi.
Polisi wakiwa kwenye mapambano.
“Sisi wakazi wa hapa palipotokea mapigano tunajiuliza, kwa nini polisi wameshindwa kutuambia ukweli wale ni akina nani badala ya kusema majambazi.
“Tangu lini majambazi wanapiga kambi mahali? Mimi ninavyojua, majambazi hufanya uhalifu na kurudi makwao. Tena naamini majambazi tunapanga nao nyumba tunazoishi au tunaishi nao mtaa mmoja au jirani,” alisema Almasi, mkazi wa Kijiji cha Kilomoni.
PILI
Wakazi hao walikwenda mbele zaidi na kusema kuwa, tangu Tanzania ipate uhuru haikuwahi kutokea majambazi wakapambana na polisi halafu polisi wakashindwa hadi kuita wanajeshi na wasikamatwe hata mmoja?
TATU
Wakazi hao waliendelea kudai kuwa, wamesikia tetesi zinazodai mwanajeshi aliyeuawa yalitokea makosa ya kiufundi kutoka kwa majeshi yetu lakini wanashangaa kimya cha polisi licha ya habari hizo kusambaa sana Amboni.
“Sisi tunasikia yule askari aliyeuawa ilitokana na makosa ya kiufundi kutoka kwa wenzake. Watu wengi hapa Mafuriko wanasema wamesikia hivyo, jeshi lingekanusha au kufafanua kama kuna ukweli,” alisema Mgaya, mkazi wa kijiji hicho.
WANANCHI MAPEMA NDANI
Baadhi ya wakazi walizungumza na Uwazi walisema licha ya kuwepo kwa polisi maeneo hayo lakini wanalazimika kuingia ndani mapema kwani kuna minong’ono kuwa, wahalifu hao wamejipanga kurudi na nguvu mpya baada ya kwenda kukutana na wenzao kwenye nchi jirani lakini jeshi la polisi mkoani hapa limekanusha uvumi huo na kuwataka wananchi waendelee na shunguli zao za kila siku.
Magaidi wa Al-Shabaab.
AL- SHABAAB ALIYEKIMBILIA KANISANI DAR...
Wakati huohuo, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Shaban, mwenyeji wa Iringa ambaye alikiri kanisani kupewa mafunzo ya kigaidi nchini Afghanistan ili kwenda kutumika na Kundi la Al-Shabaab nchini Somalia ametoweka.
Akizungumza na Uwazi, Mchungaji wa Kanisa la Victoria lililopo External-Ubungo jijini Dar, John Said alisema Shaban alifika kanisani kwake mwaka jana na kutoa ushuhuda mzito kwamba yeye na Watanzania wenzake wawili walipelekwa Afghanistan kwa ajili ya mafunzo ya dini lakini walipofika wakakuta ni mafunzo ya kigaidi.
“Shaban alitoweka, haji tena kanisani kama zamani. Alipokuja kwa mara ya kwanza alitoa ushuhuda huo mzito lakini baadaye akakata mguu,” alisema mchungaji huyo.
Katika ushuhuda wake, Shaban alisema kuwa, baada ya kufuzu walipelekwa Somalia kuungana na Al-Shabaab na kupigana na majeshi ya serikali ya nchi hiyo kwa kutumia silaha nzito lakini mwishowe aliamua kutoroka kurudi nchini.
Anasema: “Siku moja katika mapambano na majeshi ya serikali nilishuhudia wale wenzangu wawili wakiuawa kwa risasi, mimi nikatoroka katika eneo la mapigano kwa kuruka ukuta, ndiyo nikarudi hapa nyumbani Tanzania.”
UWAZI LAZUNGUMZA NA CHAGONJA
Baaada ya gazeti hili kuchimba yote hayo, lilimtafuta Kamishna wa Oparesheni ya Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Paul Chagonja ambapo alipopatikana na kumsimulia mambo yote mpaka ya Shaban, alisema:
“Mimi niko nje ya nchi kwa kazi ya kitaifa, wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (Juma Ndaki) akupe maendeleo ya oparesheni yetu kule. “Kuhusu huyo Shaban, nawasiliana na kitengo cha intelejensia sasa hivi ili atafutwe mpaka apatikane. Si yeye tu msako mkali unaendelea kwa umakini juu ya watu hao.”Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga alipotafutwa juzi, simu yake ilikuwa hewani lakini hali ya hewa ilikuwa mbaya hivyo kukosa usikivu.
0 comments:
Post a Comment