2015-02-25

Wanajeshi 6 wa JTK Waliotaka Kuandamana Wafikishwa Mahakamani Chini ya Ulinzi Mkali


Wahitimu sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali.

Washitakiwa hao ni Mwenyekiti wa Umoja wa wahitimu hao George Mgoba, Makamu Mwenyekiti Parali Kiwango, Katibu Linus Steven na wahitimu wengine Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.

Wote walikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi yao.

Walifikishwa mahakamani hapo asubuhi na kupandishwa kizimbani saa 10 kasoro jioni, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kutenda kosa la jinai.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga akisaidiwa na Tumaini Kweka, Hellen Moshi, Janethroza Kitali na Inspekta Jackson Chidunda, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi kuwa Februari 15 mwaka huu katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala Dar es Salaam, washitakiwa walipanga njama za kutenda kosa. 

Alidai siku hiyo katika eneo hilo, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lingesababisha uvunjifu wa amani. 



Katika mashitaka yanayomkabili Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT, kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

Walikana mashitaka yanayowakabili na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika. DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washitakiwa hao, chini ya kifungu cha 148 (4) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hakimu Moshi alisema washitakiwa watarudi rumande hadi Machi 6 kesi itakapotajwa kwa kuwa DPP amefunga dhamana yao kwa muda mpaka atakapoona inafaa, hivyo Mahakama haiwezi kutoa masharti ya dhamana.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Parali Kiwango (25) mkazi wa Temeke Mikoroshini alijisalimisha Makao Makuu ya Polisi, kwa Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi.

Amri ya kumtaka kiongozi huyo kujisalimisha ilitolewa juzi na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...