Dar es Salaam. Wakati kesi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ ikipangwa kusikilizwa Machi 10, klabu hiyo imesema itaiomba mahakama kuisikiliza upande mmoja endapo mchezaji huyo atashindwa kwa mara nyingine kutokea mahakamani.
Yanga ilimfungulia kesi Jaja kwenye Mahakama ya Kazi ikimdai fidia ya Sh 1.6 bilioni kwa madai ya kukiuka makubaliano ya mkataba. Jaja aliyeondoka Yanga kurudi kwao, Brazil hakutokea mahakamani kesi yake iliposikilizwa kwa mara ya kwanza jana.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha aliliambia gazeti hili jana kuwa, kesi hiyo imesogezwa mbele hadi Machi 10 kufuatia mlalamikiwa, Jaja kutokutokea mahakamani wala wakili wake wakati kesi yake ikisikilizwa.
“Kesi ilikuwa isikilizwe kwa mara ya kwanza katika hatua ya usuluhishi, lakini mlalamikiwa hakutokea mahakamani wala kutuma wakili licha ya kutumiwa hati ya kuitwa mahakamani, hivyo kusababisha isogezwe mbele.
“Baada ya kutofika mahakamani, uamuzi uliofikiwa ni Jaja kutumiwa kwa mara nyingine hati ya kuitwa mahakamani ili kusikiliza madai yanayomkabili, tutatekeleza jukumu hilo kwa njia ya EMS, Email na tutawapa nakala watu wa ubalozi wa Brazil nchini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment