BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva kumshauri Rais Jakaya Kikwete, kusitisha mchakato wa uandikishaji wapigakura kwa mfumo wa BVR.
Wamemtaka Jaji Lubuva asikubali Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfia mikononi kwa sababu kinaelekea huko na kinatafuta wa kufa naye.
Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa Dar es Salaam, Esther Samanya, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wameamua kumwandikia barua Jaji Lubuva kutokana na umuhimu wa mchakato huo unaotarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Alisema katika barua hiyo ambayo wameiwasilisha jana, wamemtaka Jaji Lubuva kufuata ushauri wao kama mzee mwenzao na afikirie upya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, badala ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.
“Kama mzee mwenzetu, tusingependa kuona historia ya nchi hii inakusuta kwa kuwazuia kujiandikisha wote pale wanapotaka kujiandikisha kwa mfano uliotokea Mkoa wa Njombe.
“Tunakuomba kama wazee wenzako, umshauri Rais Jakaya Kikwete ifikapo Aprili 30, kazi ya uandikishaji wapigakura nchi nzima itakuwa haijamalizika kwa maeneo ambayo hawajaandikisha na hawajui ni lini watawafikia, ni vyema ukalitangazia taifa mapema ili kuondoa hofu ambayo imetanda miongoni mwa wananchi,” alisema.
Samanya alisema baraza lao limeona kura ya maoni haiwezekani kufanyika tarehe iliyopangwa kutokana na ufinyu wa vifaa ambavyo havitoshelezi kukidhi haja ya wananchi wengi.
“Pamoja na uchache wa vifaa, tumeona kuna changamoto nyingi ambapo tumeshuhudia watumishi wakishindwa kutumia mashine hizo kama inavyotakiwa.
“Aidha mashine hiyo pia inashindwa kumtambua mtu aliyepaka mafuta mengi kwenye vidole vyake wakati wa kuweka alama za vidole, na pia kama seli zako zimekuwa nyingi, hasa kwa upande wa sisi wazee, inashindwa kutambua,” alisema Samanya.
Pamoja na mambo mengine, Samanya alimtaka Jaji Lubuva kuupeleka mchakato huo hadi watu wote watakapojiandikisha, kwani kwa muda huu haiwezekani watu wote wakajiandikisha na kumalizika.
0 comments:
Post a Comment