2015-03-25

Kaburi la albino lafukuliwa kagera


WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera kwa kosa la kukutwa na mifupa mitatu pamoja na nywele za mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) aliyefariki mwaka 2006 na kaburi lake kufukuliwa mwaka 2008.

Viungo hivyo vinadaiwa kuwa ni vya marehemu Zeulia Jestus (24), aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Rushwa, Kata ya Mushabago, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambapo ilifahamika kuwa alifariki mwaka 2006 muda mfupi baada ya kujifungua katika zahanati ya kijiji.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika Kijiji cha Kyota wilayani Muleba baada ya polisi kuwawekea mtego walipokuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.


Viungo hivyo wanadaiwa kuvipata baada ya kufukua kaburi la marehemu huyo mwaka 2008 na kuvitunza kwa ajili ya kuviuza ambapo wamekuwa wakiuza zaidi nywele, huku wakiendelea kusaka wateja wa mifupa.

Kamanda Mwaibambe aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Rutozi (66) aliyekuwa akihifadhi viungo hivyo na Emmanuel Kaloli (50) aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo, wote wakazi wa Kimwani.

Alisema baada ya kupata taarifa ya kuwapo watu wanauza viungo hivyo kwa bei ya Sh milioni 3, waliweka pesa za mtego na kujifanya wao ni wateja, ndipo walipofanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wawili wakiwa na mfupa mmoja na walipopekuwa majumbani kwao, walinasa mifupa mingine miwili pamoja na nywele.

“Baada ya kupata maelezo kutoka kwa watuhumiwa tulilazimika kufukua kaburi walililotaja kuwa ndiko walikopata viungo hivyo, tuliomba kibali mahakamani ili kufukua kaburi hilo na Machi 23, mwaka huu tulipofanikiwa kufukua tulikuta maiti iliyokuwa imezikwa haina viungo zaidi ya kichwa tu,” alisema Kamanda Mwaibambe.

Alisema Jeshi la Polisi linamsaka mganga wa jadi anayetambulika kwa jina la Mtalemwa Revocatus ambaye ametoroka kabla hajakamatwa kutokana na kutajwa na watuhumiwa hao kuwa ndiye aliyewapa dawa ya kinga wakati wa kufukua kaburi hilo ili wasidhurike.

Kamanda Mwaibambe alisema mwaka 2008 wananchi wa Mushabago walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuwa kaburi alilozikwa marehemu Zeulia limefukuliwa na watu wasiojulikana.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...