Serikali imesema kuwa ina haki ya kuwahamasisha wananchi kuipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa ndio iliyohusika kuiandaa.
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu alisema hiyo ni sehemu ya kazi ya serikali, lakini pia ame wataka viongozi wa dini wafanye kazi yao ya kuhubiri dini na sio kuingilia masuala ya kisiasa.
Mwalimu aliliambia Bunge kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambao walibaki kutunga Katiba walionelea kuwa muundo wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na iliyokuwa Tume ya Kutunga Katiba haikupendekezwa na wananchi walio wengi.
Alisema wananchi wengi walitoa maoni yao kwenye masuala ya afya, elimu na kilimo na ndio maana wajumbe wa BMK waliona mfumo wa serikali mbili uendelee kama ilivyo sasa.
“Kama mlikuwa mnataka serikali tatu mngebaki ndani ya Bunge la Katiba, lakini mliondoka na sisi tuliona serikali mbili ndio wananchi wanayotaka,” alisema.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema) ambaye katika swali lake alieleza kuwa muundo wa serikali tatu ndio ulikuwa unaondoa mgogoro wa namna Zanzibar na Bara wanavyoweza kutoa marais wa muungano kwa zamu.
Mnyika alisema kwamba lakini kwa bahati mbaya Katiba Inayopendekezwa ina muundo wa serikali mbili ambao kamwe hauwezi kuondoa kero na malalamiko hayo ya lini Zanzibar au Tanzania Bara itoe mgombea urais wa muungano.
Mnyika alihoji inakuwaje Serikali inakuwa na haki ya kuwahamasisha wananchi waipigie kura ya ndio Katiba Inayopendekezwa ambayo ina kasoro nyingi; lakini inawazuia viongozi wa dini pamoja na Ukawa kuhamasisha wananchi wapige kura ya hapana.
Spika wa Bunge Anne Makinda baada ya Mnyika kuuliza swali hilo aliingilia kati na kusema kwamba Ukawa hawatambuliki kikatiba na kwa upande wa viongozi wa dini alisema hawatakiwi kuhubiri siasa kwenye madhabahu ya kanisani.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Hashim Ayoub , Mwalimu alisema Serikali haina dhamira ya kufanya marekebisho ya Katiba kuhusu utaratibu wa kupata viongozi wa nafasi ya urais kwa zamu kwa kuzingatia pande mbili za muungano kwa sababu suala la uchaguzi wa rais ni suala la kidemokrasia.
Mwalimu alisema kwa mujibu wa misingi ya demokrasia wananchi wanayo haki ya kumchagua mtu yeyote kutoka sehemu yoyote ya Tanzania ambaye amekidhi vigezo vilivyoainishwa katika ibara ya 39 ya Katiba.
“Hivyo jaribio lolote la kubana wigo huu wa demokrasia itakuwa ni kinyume na misingi ya demokrasia.”
Alisisitiza kuwa utaratibu wa upatikanaji wa Rais wa Muungano umeainishwa katika Katiba ya mwaka 1977 na kufafanuliwa na sheria ya uchaguzi toleo la mwaka 2002.
Alisema sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Rais wa muungano zimeainishwa katika ibara ya 39 ya katiba hiyo. Katika swali lake la msingi, Ayoub alisema baada ya kumalizika kipindi cha Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alitoka upande wa Zanzibar ambayo ni sehemu moja ya muungano hakuchaguliwa kiongozi mwingine katika ngazi hiyo kutoka upande huo.
Alisema suala hili ni kilio kikubwa kwa Wazanzibari na lina umuhimu wake katika kuendeleza na kudumisha misingi ya muungano wetu na hasa katika mwaka huu wa uchaguzi wa Oktoba 2015.
Aliongeza kuwa hata Katiba ya Muungano haizungumzii suala la kuweka utaratibu wa kuruhusu pande hizi mbili kupata viongozi kwa zamu. Alihoji ni lini Serikali itafanya marekebisho katika Katiba ya Muungano ili kuweka utaratibu wa kupata viongozi kwa zamu.
0 comments:
Post a Comment