Utata umegubika uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi baada ya Serikali kutaka kuwasilisha ‘kinyemela’ muswada wa uanzishwaji wa Mahakama hiyo, kwenye Mkutano huu wa 19 wa Bunge unaondelea mjini Dodoma bila kuupitisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kama utaratibu unavyotaka.
Pamoja na utata huo, kwa mujibu wa ratiba ya Bunge iliyotolewa jana, muswada huo utawasilishwa kwenye kikao cha mwisho cha Mkutano huu Aprili Mosi, saa chache kabla ya hotuba ya Waziri Mkuu ya kuahirishwa kwa Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Bunge, muswada huo utawasilishwa Jumatano ya Aprili Mosi, mwaka huu baada ya kipindi cha maswali na majibu na umewekwa kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014.
Alipoulizwa ikiwa muswada huo utapata nafasi ya kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema kwa kifupi: "Muulize Katibu wa Bunge, mimi sipangi ratiba ya Bunge."
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, hakupatikana kwa maelezo kuwa yuko nje ya ofisi kikazi.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambao wanapinga kuwasilishwa kwa muswada huo, alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo.
Naye Waziri wa Uchukuzi ambaye pia anakaimu nafasi ya Waziri Mkuu, Samuel Sitta, alisema kura ya maoni iko pale pale na kwamba msimamo wa Maaskofu ‘hauna’ nguvu kwa kuwa nao wamegawanyika kwa maelezo kuwa wapo wanaounga mkono kura ya maoni na wapo wanaopinga.
Alisema viongozi hao wa dini wanapaswa kuwaacha wananchi waamue wenyewe kuhusu Katiba inayopendekezwa hivyo suala la Mahakama ya Kadhi na Kura ya Maoni, linapaswa kuamuliwa na Watanzania wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala, Jasson Rweikiza, amesema kuwa kamati yake haijapokea muswada huo na kuupitia.
Akizungumza na gazeti la Nipashe jana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema inashangaza serikali kutaka kuuwasilisha muswada huo bungeni kinyemela bila kuuwasilisha kwenye Kamati.
Alisema awali kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, Kamati ilipokea maoni ya wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi za Kiislamu na viongozi wa dini za Kikristo, ambao walionyesha kasoro nyingi kwenye muswada na hivyo Kamati iliiagiza serikali ikafanye marekebisho na kuyawasilisha kwake kabla ya kupeleka bungeni.
“Sisi (Kamati), ndiyo wenye muswada na tulikuwa hatujakubaliana, tukawaambia serikali tupate kwanza maridhiano ya jambo hili kwa sababu tulipokea maoni ya wadau wengi ambao walibaini makosa na kasoro za kitaalam; serikali ikaahidi kuyafanyia kazi lakini hadi leo hawajarudi kwenye kamati kutuletea marekebisho, sasa tunashangaa wameuweka kwenye ratiba ya Bunge,” alisema.
Alisema ni hatari kwa mambo yanayoweza kuligawa taifa kama uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi na Katiba inayopendekezwa kufanywa kwa hila na ubabe na kuishauri serikali ihakikishe wananchi wameelewa kwa kina jambo hilo ili kuepuka mgawanyiko usio wa lazima.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Ofisi za Bunge, zinaeleza kuwa muswada huo unaweza kusomwa kwa mara ya pili ukiwa sehemu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014.
Chanzo chetu kilieleza kuwa hata hivyo, kuwasilishwa kwa Muswada wa Mhakama ya Kadhi kutategemea makubaliano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusiana na mambo gani yawasilishwe.
Utata huo umeibuka takribani mwezi mmoja baada ya Serikali kuuchomoa muswada huo bungeni kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge iliofanyika Februari, kwa nia ya kutafuta maridhiano kwanza.
Aidha, taasisi 11 za Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ziliazimia kuwahamasisha wana jumuiya wake kususia Kura ya Maoni ya Katiba Mpya hadi watakapopata uhakika wa kuwa na Mahakama ya Kadhi yenye meno.
Baada ya serikali kuuchomoa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana Dodoma na serikali iliomba muda wa kufanya maridhiano kabla ya kuwasilishwa muswada huo kwenye Bunge hili.
Mbali ya maridhiano, Kamati hiyo ilitaka muswada huo uwasilishwe wenyewe badala ya kuingizwa kwenye muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2014, jambo ambalo hata hivyo, halijafanyika kwa kuwa umewasilishwa ukiwa kwenye muswada wa sheria mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment