2015-03-13

Tume Ya Uchaguzi Yasema Haiwezi Kutengua Ubunge Wa Zitto Kabwe Hadi Ipokee Barua Ya Spika wa Bunge na Sio ya CHADEMA Pekee.



Tume ya Uchaguzi imesema hata ikipokea barua kutoa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe haina uwezo wa kuchukua hatua yoyote mpaka watakapopokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge.


Akizungumza na mwandishi, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham, alisema mpaka sasa hakuna barua iliyofika katika ofisi hiyo kutoka Chadema na hata kama ikifika Tume ya Uchaguzi haitatoa uamuzi wowote mpaka watakapokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge ambaye kisheria yeye ndiye anayetoa taarifa kama kuna jimbo lipo wazi.

Alisema kwa tukio hilo la kuvuliwa uanachama kwa Zitto ni lazima barua ya Spika ifike ikitangaza kuna jimbo liko wazi ndio Tume ya Uchaguzi wanaweza kufanya maamuzi na sio barua ya chama au mtu yeyote kutoka chama chochote.

Aliongeza kuwa kisheria mwenye mamlaka ya kutaarifu Tume masuala ya nafasi iliyopo wazi ni Spika wa Bunge pekee na hawawezi kutumia habari zilizopo kwenye vyombo vya habari na kuchukua maamuzi.

“Lazima tupate barua ya Spika ikitangaza kama kuna eneo ambalo mbunge wake amevuliwa uanachama , amefariki, au ana matatizo ambayo yanamfanya ashindwe kuendelea kuwa mbunge,” alisema Masham.

Wiki hii, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na Zitto dhidi ya chama chake.

Jaji Richard Mziray alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi la awali lililowasilishwa na Chadema kupitia mawakili wake Peter Kibatala, Tundu Lissu na John Mallya ambao walidai kesi hiyo ilifunguliwa bila kufuata utaratibu wa sheria.

Aidha, Tundu Lissu ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema alisema: “Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, mwanachama yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama chake, endapo atashindwa katika kesi hiyo atakuwa amejiondoa uanachama wake, kwa hiyo natangaza rasmi Zitto Kabwe sio mwanachama tena wa Chadema."

Kuhusu utambulisho wa Zitto bungeni, Lissu alisema kwa mujibu wa kanuni za chama chake, Katibu wa chama chake anatakiwa kumwandikia barua Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kumjulisha Zitto tena si mwanachama wao na taratibu zingine zitafuata.

Naye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, amebainisha kuwa endapo Bunge litapata taarifa rasmi ya Chadema kumvua uanachama Zitto, lazima Bunge hilo lifanye kwanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo litoe uamuzi.

“Si lazima Spika akubaliane na uamuzi wa kutengua ubunge wa mbunge husika kwani kama haikuwa halali kwa mbunge huyo kuvuliwa uanachama, Spika hubatilisha uamuzi wake wa kumvua ubunge mhusika,” alisema Kashililah.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...