2015-03-05

Wastaafu Bandari watafuta huruma ya Waziri Sitta


Na Burhani Yakub, Mwananchi


Tanga. Wastaafu 263 wa iliyokuwa Mamlaka ya Bandari nchini (THA) wamemwomba Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kuingilia kati mgogoro wa muda mrefu wa kulipwa mafao yao ya Sh2 bilioni.


Wafanyakazi hao walistaafishwa kazi tangu Juni 30, 1997 wakiwa katika Bandari ya Tanga.


Walisema fedha hizo ni malimbikizo ya mapunjo yao tangu Julai 1997 hadi 2002, mkono wa kwa heri pamoja na makato yaliyofanyika kinyume na utaratibu.


Kiongozi wa kufuatilia madai hayo, Augustino Sekihola akizungumza na gazeti hili jana alisema wameamua kumwomba Waziri Sitta aingilie kati baada ya kuona wanazungushwa bila kulipwa haki yao. Kiongozi huyo alisema wastaafu hao wanaamini kwamba Sitta atakamilisha kazi iliyoanzwa kufanywa na mtangulizi wake, Dk Harrison Mwakyembe ambaye kwa sasa amehamishiwa katika Wizara ya Afrika Mashariki.


“Tulishaonana na Mwakyembe lakini kabla ya kufanikisha suala letu, alihamishiwa akatushauri tumuone Sitta akiamini kwamba atatusaidia na tutalipwa haki zetu,” alisema Sekihola.


Amina Rajabu alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ambayo ilibadilishwa jina kutoka iliyokuwa THA wamekuwa wakisuasua kutoa malipo yao wakati inafahamika wazi kwamba walipunjwa.


“Tumefuatilia kwa muda mrefu sasa hadi wenzetu wametangulia mbele ya haki, huku TPA ikiziba masikio na kujifanya haijui,” alisema Amina. Kaimu Meneja wa TPA Tanga, Fred Liundi alipoulizwa kuhusu madai ya wastaafu hao alisema hawajawahi kufika ofisini kwake wala kwenye kumbukumbu hakuna barua waliyowasilisha ya kudai mafao hayo.


Hata hivyo, alisema ofisi ya yake iko tayari kukaa na kusikiliza madai yao ili waone kama yana msingi na yashughulikiwe.


“Nipo tayari kukaa nao na kuwasikiliza, nashauri waje tukae ili tuweze kuangalia kwa pamoja madai yao, hawajawahi kuja wala kuleta madai hayo kwa maandishi,” alisema Liundi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...