2015-02-02

Kesi ya Ponda kusikilizwa leo



Shahidi wa pili ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Morogoro (RCO) Jafert Kibona ambaye amehamishiwa Mtwara.

Morogoro. Kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, inaendelea kusikilizwa leo kwa shahidi wa tatu kutoa ushahidi wake.

Katika kesi hiyo yenye mashahidi 15 wa upande wa mashtaka, Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kutotii amri halali ya Mahakama, kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa. 


Makosa hayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10, 2013 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) Sadick Tindwa ambaye amehamishiwa Handeni mkoani Tanga.

Shahidi wa pili ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Morogoro (RCO) Jafert Kibona ambaye amehamishiwa Mtwara.

Wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa Sheikh Ponda bado yuko rumande kutokana na Mahakama hiyo kushindwa kumpa dhamana kutokana na hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kuzuia kwa masilahi ya Taifa.

Mawakili wanaomtetea Sheikh Ponda ni Juma Nasoro, Bathoromeo Tarimo na Abubakar Salim. 


Upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali Kanda ya Mashariki, Benard Kongola, Sunday Hyra na George Mbalasa.

Kesi hiyo imekuwa ikiendeshwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...