SIRI mpya juu ya Mtanzania Rashid Charles Mberesero, anayehusishwa na tukio la kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya zimeibuka.
Kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari vya Kenya, Mtanzania huyo anayedaiwa kuwa miongoni mwa magaidi wa Al-Shabaab walioua watu 148 katika chuo hicho, endapo angesalimika baada ya tukio hilo, angepelekwa Somalia yalipo makao makuu ya kundi hilo la kigaidi.
Hayo yalibainishwa jana na mwendesha mashtaka wa nchi hiyo, Daniel Karuri katika mahakama ya jijini Nairobi.
Mahakama hiyo imeamuru Rashid akae kizuizini kwa siku 30 akisubiri uchunguzi wa tuhuma zake.
Pia watu wengine 14 wanaotuhumiwa kuhusika na kundi la Al Shabaab wameamuriwa wakae rumande kwa muda wa siku 30 wakisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Polisi inaendelea kuchunguza mawasiliano ya simu waliyokuwa wakifanya watuhumiwa hao kwa ajili ya kutafuta ushahidi zaidi wa wahusika wote wa shambulio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka husika, Rashid alikamatwa akiwa amejificha juu ya dari la chuo hicho akiwa ameshikilia silaha na mlipuko.
Mmoja miongoni mwa watuhumiwa hao alikamatwa katika chuo kikuu hicho, akiwa anafanya kazi kama mlinzi na wengine walikamatwa wakati wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia Somalia.
Wakati walipovamia chuo hicho, wauaji waliwatenga wanafunzi wa Kiislamu na wale waliobainika kuwa Wakristo waliuawa kwa kupigwa risasi.
Kundi la Al Shabaab limedai kuhusika na mauaji hayo na kwamba tukio hilo lilidhamiria kutuma salamu kwa Serikali ya Kenya ambayo imehusika kutuma majeshi yake Somalia kupambana na kundi hilo.
Mara ya mwisho kwa Kenya kushambuliwa ilikuwa mwaka 1998 ambako ubalozi wa Marekani ulilipuliwa jijini Nairobi.
MIEZI MITANO NJE YA SHULE
Mama mzazi wa Rashid, jana alilieleza gazeti hili kuwa wakati Mkuu wa Shule ya Bihawana, Mbilinyi Joseph akisema tangu Novemba mwaka jana mtoto huyo alitoroka shuleni, yeye anajua mwanawe huyo kwa kipindi cha mwisho wa mwaka alibaki shule ili asome masomo ya ziada.
“Wakati huyo mwalimu wake akisema kuwa Rashid hayupo shuleni kuanzia Novemba, nakumbuka kuwa huo mwezi alinipigia simu akaniambia kwa sababu yeye alichelewa kuanza masomo, anataka abaki shuleni ili asome tuisheni awafikie wenzake.
“Akaniambia nimtumie hela ya twisheni, nikamtumia Sh 110,000 ili Sh 60,000 iwe ya tuisheni na nyingine ya kunua viatu na mahitaji yake mengine.
“Kwa hiyo muda wote huo nilikuwa najua mtoto yuko shuleni na ilivyofika mwezi wa tatu ndiyo akaja nyumbani akaniambia wenzao wa kidato cha sita walikuwa wanafanya mtihani na baada ya hapo kulikuwa na likizo ya wiki.
“Alisema hakuona sababu ya kusubiri hadi shule ifungwe kwa sababu wakati huo wenzao wakifanya mtihani, wao hawakuwa wakisoma, kwa hiyo ameamua kurudi nyumbani,” alisema.
Alisema katika kipindi ambacho mwanawe huyo alikaa nyumbani, hakuhisi mabadiliko yoyote ya tabia yake na kuwa alimsaidia kuvuna mazao yake shambani.
“Kabla ya Pasaka ndiyo akaniambia kwa kuwa umebaki muda mfupi shule ifunguliwe na kwa sababu yeye ni Muislamu hana sababu ya kusubiri sherehe za Pasaka, anarudi shuleni ili akaendelee na masomo.
“Sasa nashangaa kusikia kwamba hakuwepo shuleni tangu mwezi wa 11, kwanini hao walimu hawakunipigia simu kuniambia hadi tunasikia hayo ya Kenya namtuma shangazi yake ndiyo wanamwambia muda mrefu mtoto hakuwa shuleni?” alihoji mama huyo.
Alisema wakati huo wa mwisho wa mwaka jana alipokuwa akijua kuwa mwanawe yupo shuleni, alikuwa akiwasiliana naye ingawa siyo mara kwa mara.
“Alikuwa ananipigia simu, lakini alikuwa anatumia namba tofauti tofauti kwahiyo sikuziweka na nilijua tu anaomba simu za walimu wake kwa sababu pale shuleni hawaruhusiwi kuwa na simu.
“Kwahiyo mimi kabisa nilijua mtoto wangu yupo shule na aliniahidi atasoma kwa bidii hadi awafikie wenzake ambao tayari walikuwa wamemtangulia,” alisema.
MWALIMU MLEZI AFUNGUKA
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Bihawana, ambaye pia ni mlezi msaidizi wa Kikundi cha Waislamu cha Tamsiia cha shuleni hapo, Idd Hussein, jana aliliambia gazeti hili kuwa Rashid alihamia mwaka jana kutoka Shule ya Sekondari Kigwe iliyoko Wilaya ya Bahi.
“Huko Kigwe alikuwa anasoma mchepuo wa HGL, alipokuja hapa akabadili akawa anasoma PCB… Alikuwa ni mtu mwenye misimamo na alishikilia sana dini,” alisema.
Alisema Rashid alikuwa anapenda kwenda msikitini, akifika alikuwa anasali na akimaliza anasoma Quran kidogo na kurejea bwenini kuendelea na taratibu zake nyingine.
Mwalimu Hussein alisema kutokana na shule hiyo kuwa ya mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu ni marufuku kuvaa rozari wala balaghashia.
“Rashid alikuwa ni mbishi, alivaa balaghashia maeneo ya shule hali iliyosababisha atofautiane na mkuu wa shule ikamlazimu atuite tuzungumze nae.
“Mkuu wa Shule alitaka kuichana balaghashia lakini tukamsihi asifanye hivyo kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuleta chuki kwa Waislamu hivyo tukashauri ampe adhabu ambayo hata hivyo hakuifanya badala yake akapotea shuleni,” alisema.
Alisema baada ya Rashid kupotea shuleni hapo, yeye na viongozi wenzake walimuita kiongozi wa wanafunzi wa Jumuiya ya Kiislamu shuleni hapo ambaye alidai hajui alipokwenda kwa kuwa hakumuaga.
KAULI YA RPC, DC
Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Dodoma, David Misime alipoulizwa kuhusu kijana huyo kutokea Sekondari ya Bihawana, alisema hawezi kuliongelea suala hilo.
“Ugaidi umefanyika Kenya sio Dodoma kwa hiyo siwezi kuliongelea suala hilo,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya (DC) ya Dodoma Mjini, Betty Mkwasa alisema hana habari kwamba Rashid alikuwa anasoma Sekondari ya Bihawana.
“Mie sina taarifa ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, basi ngoja nilifuatilie,” alisema Mkwasa.